MTUME WA UISLAAM NI KIONGOZI BORA WA VIUMBE

MUHADHARA WA MHESHIMIWA AYATULLAHIL-UDHMA SAYYID SWAADIQ SHIRAZI

(Mungu amzidishie umri)

 

Kwa jina la Mwenyezi Mungu mwingi wa rehma mwenye

Kurehemu.

Sifa zote njema ni zake mola wa viumbe wote na rehma na amani ziwe juu ya Muhammad na aali zake watwaharifu, na laana ya daima iwe juu ya maadui zao wote hadi siku ya ufufuo.

 

WATU WALIINGIA VIPI KATIKA UISLAAM MAKUNDI KWA MAKUNDI?

Mtume wa uislaam  (s.a.w.w) alikaa na kubakia katika mji mtukufu wa Makkah, kwa muda wa miaka kumi na mitatu takriban baada ya kupewa utume mtukufu, kisha baad ya hapo akahamia katika mji wa Madinatul-munawwarah, na kubakia huko hadi alipo kufa shahidi (s.a.w.w) kwa kulishwa sumu katika siku  kama ya leo (Tarehe ishirini na nane ya mwezi wa Safar 28).

Na katika kipindi cha miaka hii kumi na tatu, ambayo Mtume mtukufu (s.a.w.w) aliishi na kukaa katika mji mtukufu wa Makkah, baada ya kupewa kwake utume, wanahistoria wametaja idadi ya wale watu ambao waliingia katika uislaam ambao walikuwa ni zaidi ya watu mia mbili.

 

MTUME ALIUTEKELEZA UISLAAM  KIMATENDO

Ama kipindi alicho kuwa katika mji wa Madinatul-munawwarah Mtume (s.a.w.w) aliutekeleza uislaam kimatendo, na hapo watu wakawa wakiingia kwenye uislaam makundi kwa makundi hadi Mwenyezi Mungu akasema ndani ya Qur’an tukufu:(Na ukawao watu wakiingia katika dini ya Mwenyezi Mungu makundi kwa makundi)(Suuratun-nasri aya 2). Katika kipindi hiki kifupi ambacho Mutme alikimaliza akiwa Madina, Maelfu kwa maelfu ya watu waliingia katika uislaam, na yote hayo yalifanyika na kupatiakana katika kipindi cha miaka miwili au mitatu ya mwisho ya umri mtukufu wa Mutme (s.a.aw.w) sasa ni vipi jambo hili liliweza kuthibiti na kuwa?

Hakika Mtume mtukufu (s.a.w.w) ndie mtu na shakhsia  kubwa na mtu bora alie umbwa na Mwenyezi Mungu mtukufu, kwani  hata Imam Amiril-muuminiin Ali bin Abi Twalib (a.s) alipoulizwa ya kuwa (wewe ni bora au Muhammad) akasema: (Mimi ni mtumwa kati ya watumwa wa Muhammad). (Al-kafiy juzu 1/ 89).

 

KANUNI  NA SHERIA ZA UISLAAM  NDIO KANUNI BORA NA ZILIZO KAMILIKA KULIKO KANUNI ZOTE

Hakika sunna au nidhamu na hukumu pia kanuni  ambazo ziliwekwa na Mtume wa uislaam (s.a.w.w) kwa waislaam, mfano wake ni sawa na Mtume mwenyewe, kwani kanuni hizo ni baora na zilizo kamilika kuliko kanuni na hukumu zingine zote, na ni wajibu na lazima iwe hivyo, kwa maana kuwa nilazima kuwe na uwiano na kuto pingana kati ya usuul na furuu’u, na hili ni jambo lililopo.

Ukweli ni kuwa muda wote aliokuwapo mtume wa uislaam (s.a.w.w) katika mji wa Makkah, baada ya kupewa utume mtukufu, ratiba na barnamiji zake  na mafunzo yake na siasa zake hazikutoka na kutangazwa wazi wazi, maneno yake hayakutekelezwa kimatendo, kwani bado  maandalizi na mazingara ya kuweza kuyatekeleza yalikuwa bado hayajatengamaa, na Mtume (s.a.w.w) hakuwa na uwezo na nyezo ya aina yoyote wala hakuna na hiyari ya aina yoyote, mpaka afahamishwe namna gani ataweza kutendeana na kufanyakazi na watu:

-Vipi ataamiliana na wasaidizi wake (Answari wake) na maadui zake?

-Namna gani  atazitumia mali?

-Namna gani ataweza kupigana vita? Na baada ya vita atafanya nini?

-Ni nidhamu ipi au mfumo upi atakao utangaza kwa watu?

-Ni barnamiji ipi atakayo itekeleza yeye mwenyewe (s.a.w.w) kimatendo?

 Lakini yote hayo yalibainika alipokuwa Madinah, na mfumo huohuo ndio ulio tekelezwa na Amirul-muuminiin (a.s), kwa muda wa miaka mitano ya utawala wake baada ya kupita miaka ishirini na tano tangu kufa shahidi Mtume (s.a.w.w).

Someni historia ya Mtume wa uislaam (s.a.w.w) ili muone mamia ya mifano hai, ambayo lau kama inge kusanywa na kujumuishwa pamoja, kwa hakika mtu yeyote yule asiekuwa muislaam hata lau kama ange kuwa ni mtu mwenye taasubi-na asiwe mpindazi-ataweza kuathirika kwa mifano hiyo, na kuingia kwenye uislaam.

Kwa hivyo basi ikiwa leo au siku yoyote ile mfumo na nidhamu pia hukumu za mtume wa uislaam (s.a.w.w)  pia hukumu za Amiril-muuminiin (a.s) zitaweza kutekelezwa katika majumba yetu, na sehemu zetu za  kazi, na katika mashirika yetu ya kazi na katika miji yetu, basi yange thibiti yale yaliyo thibiti kabla ya miaka elfu moja na mia nne, nayo ni tafsiri na taawili ya kauli ya Mwenyezi Mungu alie takasika:(Na utawaona watu wakiingia katika dini ya Mwenyezi Mungu makundi kwa makundi), na mtaona mamilioni ya makafiri wakiingia katika uislaam.

 

MFUMO WA MTUME (S.A.W.W) ULIKUWA VIPI?

Katika historia ya Mtume wa uislaam (s.a.w.w), kuna mifano na vielelezo vingi viwekavyo wazi ukweli na uhakika wa mambo tuliyo yaeleza hapo kabla. Na marehemu kaka yangu mheshimiwa ayatullahil-udhmaa Sayyid Muhammad Al-huseiniy Al-shirazi (Mwenyezi Mungu autukuze utajo wake) alikuwa akisisitiza na kuwatilia mkazo awahutubiao mara kwa mara katika mazungumzo yake na vitabu vyake, kama mlivyo sikia nyinyi pia kutoka kwake zaidi ya mara moja, ya kuwa wasome historia ya Mtume wa uislaam (s.a.w.w) ili waweze kuona iko vipi, na kwanini ilikuwa hivi, hadi Mwenyezi Mungu akasema katika Qur’an tukufu na yenye hekima (Na utawaona watu wakiingia katika dini ya Mwenyezi Mungu makundi kwa makundi)? Hakika uingiaji wa aina hii haukuwa ni muujiza na jambo lisilo la kawaida, bali hayo yalikuwa ni matokeo na natija ya kawaida ya mfumo na njia na usuluubi wa mtume wa uislaam (s.a.w.w).

Sasa ni akina nani wale ambao waliingia katika dini ya uislaam makundi kwa makundi, katika zama za Mtume mtukufu (s.a.w.w)? kwa hakika idadi kubwa ya watu hao walikuwa ni waabudu masanamu, kama ambavyo idadi fulani ya watu hao walikuwa ni wakiristo, hawakuja mtu mmoja mmoja, bali walikuwa wakija makundi kwa makundi na kuingia katika dini ya kiislaam,  na miongoni mwao ni Mayahudi pia, na hasa wale ambao walikuwa wameingia katika mji wa Madinatul-munawwarah  na waliokuwa pembezoni mwa mji wa madina, hawa ni sawa na wale waliingia katika uislaam makundi kwa makundi.

Lakini vipi waliingia katika uislaam kwa mara moja na kwa mkupuo, hadi Mwenyezi Mungu alie takasika akasema kuhusiana nao (Na utawaona watu wakiingia katika dini ya Mwenyezi Mungu makundi kwa makundi)?!

Waliona nini? Na walisikia nini?

Na ni kwa sababu ipi walikubali kusadikisha na kujiunga au kuingia katika uislaam?

Ikiwa hivi leo yatapatikana mazingira na hali kama ile, na kauli zile zilizokuwa zikisikika, na itikadi kama zile katika sehemu yoyote ya ulimwengu-sawe iwe katika nchi za magharibi au mashariki-basi watu wangeufuata uislaam kwa shauku na mapenzi, na wangekuwa waislaam, na wakati huohuo azma ya waislaam inge pata utukufu na nguvu zaidi na zaidi na itikadi zao kuimarika na kujizatiti kwa uimara, na wange fanya juhudi zenye kuendelea za kuwaongoza watu wengine.

Hakika maisha ya Mtume mtukufu (s.a.w.w) yamejawa na mifano mingi hai, someni historia yake (s.a.w.w) na idhihirisheni mifano hiyo hai ambayo ni mamia kwa mamia kwa Wakiristo na Mayahudi na Washirikina na wapingao kuwepo kwa mwenyezi Mungu (walahidi), wakati huo mtaona namna watakavyo silimu, kama ambavyo kila muislaam popote atakapo kuwa atahisi utukufu na uimara wa imani yake, na itakuwa ni sababu ya kuwaongoza watu wengine, baada ya kuyafahamu hayo.

Imepokelewa katika riwaya kwamba itakuja siku ambayo aya tukufu itageuka na kuwa kinyume chake na uhakika wenyewe utakuwa ni (Na utawaona watu wakitoka kwenye dini ya mwenyezi Mungu makundi kwa makundi) (Buharul-an’waar juzu 24 / 219), kutokana na kuutupa mkono mfumo wa Mtume mtukufu (s.a.w.w) na kuacha kumuitakidi yeye, na namtaraji Mwenyezi Mungu zisiwe ni siku zetu hizi tunazo ishi hivi leo ndio siku zile zilizo zungumziwa.

Lau kama mge tekeleza mfumo ambao ulikowapo mwanzoni mwa uislaam, katika familia zenu, hakika majirani zenu na watu wenu wa karibu na wale ambao mna mahusiano nao na mawasiliano ya kifamilia, wange pata itikadi kidogokidogo, lau kama wange kuwa makafiri wangekuwa waislaam, na lau kama wange kuwa si wenye kuwapenda Ahlil-baiti, basi wange badilika na kuwapenda na kuwa wapenzi wao (a.s) na lau kama wasinge kuwa ni watu wenye dini, basi wange kuwa ni wafuasi wa dini, na hayo ni kutokana na ukweli kuwa mfumo wa kiislaam na hukumu zake na kanuni zake ni tukufu na nzuri.

 

MFANO HAI WA KANUNI  NA SHERIA ZA DOLA LA KIISLAAM

Nitakupeni na kukutoleeni mfano mmoja hai uonyeshao njia na namna mtume alivyo kuwa akifanya kazi, na mfano huo umetajwa kwenye vitabu vya hadithi vya kishia na kisunni, na katika sahihi sita, na katika vitabu vya historia vya makafiri pia.

Riwaya hii ambayo nitainukuu na kukusomeeni lau kama watasomewa watu wa aina yoyote ile, au wafuasi wa dini yoyote ile au madhehebu yoyote yale na wa nchi yoyote katika mabara ya dunia hii bala shaka watabadilika ikiwa watawaamini na kukubali mambo hayo.

Riwaya inasema: Wakati ambapo Mtume wa uislaam (s.a.w.w) alipokuwa katika mji wa Madinatul-munawwarah, alikuwa akisimamia pia mambo mengi kwa sifa ya kuwa yeye ni raisi na kiongozi wa juu wa dola la kiislaam, Mtume (s.a.w.w) alitangaza wazi ya kuwa: Mtu yeyote atakae fariki na kuacha mali basi mali hiyo ni ya warithi wake) hiyo ina maanisha nini?  (Al-kafiy juzu 7 / 167)    

Hakika suala la (kodi ya mali ya urithi) limeenea hivi leo katika nchi nyingi za ulimwengu, bali kodi hiyo ipo na inatozwa hadi kwenye madola na nchi ambazo zinadai ya kuwa zina sheria na kanuni zilizo bora.

Hakika kanuni ya (kuitole kodi mali ya urithi) haihusu tu zama hizi za leo, bali suala hilo linarejea kihistoria kabla ya uislaam, kwani suala hilo lilikuwa limeenea kati ya washirikina. Kwa mfano katika kanuni na sheria za washirikina kabla ya uislaam-vile vile dini mbili ya ukiristo na uyahud dini zilizo potolewa-ilikuwa ikitumika sheria kama hii, pindi alipokuwa mtu fulani  akifariki na kuacha mali, basi raisi wa serikali au raisi wa kabila, au mtu yeyote mwenye madaraka na hatamu ya uongozi, alikuwa akichukua fungu fulani katika mali hii ya urithi, kama kodi juu ya mali hiyo ya urithi.

Ama katika uislaam hakuna kitu kiitwacho kwa jina la (kodo ya mali ya urithi) kutokana na kwa mujibu wa hadithi ya Mtume (s.a.w.w).

Anasema Mtume (s.a.w.w) pia: (Mwenye kufariki na kuacha deni au familia basi deni hilo ni juu yangu kulilipa  na familia hiyo ni jukumu langu kuitunza)  Yaani mtu yeyote akifariki na hakuacha mali, na alikuwa ni fakiri, na akaacha familia ambayo haina uwezo wa kujitunza na kupata mahitaji, basi (ni juu yangu na jukumu langu), yaani hakika matumizi yao ni juu Mtume (s.a.w.w) .(Kanzul-ummal juzu 11 / 10)

Na bila shaka, hakika Mtume wa uislaam (s.a.w.w) alikwenda mbali zaidi ya hapo, na mimi ninaitakidi ya kuwa hakuna kanuni na sheria kama hii katika sehemu yoyote ya ulimwengu. Na hata madola tajiri na madola ambayo yanadai kuwa yameendelea  kimiji na wananchi, hayana kanuni na sheria kama hii isemayo kuwa (Mwenye kufariki na kuacha deni au familia basi deni hilo ni juu yangu kulilipa na ni jukumu langu kuitunza familia hiyo).

 

HAKUNA MAISHA BORA NA YA RAHA ISIPOKUWA NDANI YA UISLAAM

Je kuna kanuni na sheria mfano wa kanuni au sheria kama hii, hata kwenye madola tajiri katika ulimwengu wa leo, yaani mtawala na Raisi au kiongozi wa juu achukue jukumu la kulipa deni la mtu alie fariki? Ndio pengine yawezekana ikatokea kuwepo baada ya ufuatiliji wa muda mrefu katika idara na ofisi za serikali, warithi wakaweza kupata fungu fulani la mali, lakini hakuna jambo kama hili (dhamana bima  ya deni), kama kanuni, katika sehemu yoyote ya ulimwengu.

Kuna nukta ambayo hapana budi kuizungumzia na kuielezea, nayo ni kuwa hivi leo katika baadhi ya madola na nchi kuna bima ya kijamii.

Na katika baadhi ya madola tajiri, kuna kanuni na sheria inayo iruhusu familia fukara ambayo imeondokewa na baba wa familia hiyo kupata fungu fulani la mali, lakini si kwa kiwango ambacho kinatosheleza kukidhi mahitaji ya fmilia ile.

Kisha, hata kama tutajaali ya kuwa dola au nchi moja wapo ikijitokeza na kutangaza mambo kama haya yafuatayo:

1-Sisi hatuna kodi ya mali ya urithi.

2-Ikiwa mtu atafariki na kuacha familia fukara, sisi tutachukua jukumu la kuitunza familia hiyo, na akiwa na deni tutalipa deni lake…

Je hamuitakidi ya kuwa watu wengi, kutoka sehemu mbali mbali za duni na nchi zingine za ulimwengu, wataziacha nchi zao na kuhamia kwenye nchi ile, na kuchukua uraia wa nchi hiyo na kuwa wakazi na wananchi wa nchi hiyo?

Pamoja na kuwa hakuna mfano wa jambo kama hili, isipokuwa nyinyi mnaona na kushuhudia watu kadhaa, kutoka kwenye nchi za kiislaam na nchi zinginezo, wakihamia kwenye madola na nchi ambazo kwa kiwango fulani zinahali nzuri ya kimaisha na kiuchumi na amani kwa kiwango fulani, au wanahamia kwenye nchi ambazo kwa kiwango fulani hazina ukandamizaji hata kama kwa kiwango kidogo ukilinganisha na nchi zingine, vyovyote nchi hizo zitakavyo kuwa zikifuata na kushikamana na dini.

Lakini jambo lisilo na shaka na la yakini kwa ujumla ni kuwa: Imethibiti na kuainishwa katika uislaam, juu ya imamu wa waislaam, kusimamia utoaji wa matumizi ya familia fukara, kwa kiwango kinacho tosheleza familia hiyo na kulipa madeni yao.. Imam Swaadiq (a.s) anasema: (Ni juu ya imamu kulipa deni hilo, na ikiwa hakulilipa basi ni juu yake dhambi ya kuto fanya hivyo) (Al-kafiy juzu 1 / 407, h 7).

Hakika Nabii wa uislaam (s.a.w.w) alitoa zawadi hii ya pekee na kuupatia ulimwengu, na katika zawadi hiyo kuna wema na saada ya viumbe wote.. na hili ni jambo litakalo thibiti kwa mara ya pili pale atakapo dhihiri Swaahibul-asri waz-zamaan walii mtukufu wa Mwenyezi Mungu  imamul-hujjat (Mwenyezi Mungu aharakishe kudhihiri kwake), na kuthibiti ahadi ya Mwenyezi Mungu (ili dini yake aifanye kuwa ni yenye kuzishinda dini zingine zote) (Suuratut-tawbah aya 33).

Na ni jambo la kawaida na lenye kufahamika ya kuwa makusudio ya Imamu Swaadiq (a.s) ya neno (imamu wa waislaam) si imamu maasumu, na hiyo ni kutokana na ukweli kwamba imamu maasumu hafanyi dhambi, bali makusudio yake katika neno imamu katika hadithi hii tukufu ni mtu ambae ameshika kamba ya uongozi na utawala, na mwenye kumiliki au mwenye kuwa na uwezo kama huu.

 

MAYAHUDI WANAJIUNGA NA UISLAAM

Kuna riwaya kutoka kwa imamu Swaadiq (a.s) inayowiana na yaliyo semwa na Mtume (s.a.w.w), nayo imo ndani ya vitabu vyetu, kama ambavyo riwa hiyo ni moja ya sehemu ya  hadithi zetu tunazojifakharisha nazo, kwani maimamu wetu wa Ahlil-baiti (a.s) wana vitu fulani ambavyo hakuna mtu yeyote mwenye navyo na kuvimiliki.. isipokuwa ukweli ni kuwa ni jambo la kusikitisha ya kuwa baadhi yetu  hawafahamu maimamu wetu ni mambo gani waliyo nayo na ni vitu gani walivyo navyo na vilivyoko kwa maimamu wetu..

Imamu Swaadiq (a.s) anasema: Na hakukuwa na sababu ya kusilimu mayahudi wote-au mayahudi walio wengi- isipokuwa ni baada ya kudhihiri kwa kauli hii ya Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.w) (Al-kafiy juzu 1 / 407,h7).

Wakati Mtume (s.a.w.w) alipokuwa akitekeleza majukumu na wadhifa wake, kama Raisi wa dola na serikali. Katika mji wa Madinatul-munawwarah, alitangaza na kubainisha jumla zile maalum, na kuzibainisha na kuzidhihirisha kama kanuni na sheria, na kutokana na iilani hiyo, Mayahudi wengi waliingia katika uislaam, kama so wote, na hiyo inatokana na ukweli kuwa kawaida na tabia ya mayahudi ni kuchuma na kulimbikiza mali, na baada ya kutangazwa kwa kanuni zile ikawabainikia na kufahamu ya kuwa uislaam ni dini mzuri, kwa hivyo wakapendezewa kuingia katika uislaam, na huenda wao walifikiria kama ifuatavyo: ikiwa tutakuwa matajiri na tukafariki, hakika Raisi na kiongozi huyu wa dola na serikali ya kislaam hatachukua chochote katika mali zetu, na zitarithiwa na watoto wetu na warithi wetu ikiwa kamili na bila upungufu wowote. Ama ikiwa tutakuwa mafukara, kwa hakika hakuna jambo la kututia kero katika hali kama hii pia, kwa sababu Raisi na kiongozi wa dola na serikali ya kiislaam atazipatia familia zetu matumizi ya maisha yenye kutosheleza, kama ambavyo lau kama tutafariki na kuacha madeni, hakika watu wenye kutudai hawata wafuatilia watoto wetu na warithi wetu, kwa sababu mtu huyu (Nabii wa uislaam s.a.w.w) anasema: (Madeni ni juu yangu na matumizi ya familia ni jukumu langu). Kwa hivyo, hakika Mayahudi ambao wamezungumziwa na Qur’an tukufu kwa kauli yake isemayo (Mtawakuta watu wenye uadui mkubwa kwa waumini ni Mayahudi) waliingia kwenye uislaam mtu mmoja mmoja na familia na makundi kwa makundi. (Suuratul-maaidah aya 82).

Ni kweli, hakika Mayahudi wale waliingia kwenye uislaam kwa ajili ya mali, lakini watoto wao na familia zao waliona nuru ikiwa kati ya waislaam na ikiwa kwa waislaam, na kukua na kulelewa katika himaya ya uislaam, kwa hivyo basi idadi kadhaa ya maulamaa wa kiislaam, huenda wakawa wanatokana na vizazi vile vya mayahudi wale ambao walisilimu katika siku zile.

Hayo yaliyo tangulia ni mfano hai mmoja wapo katika ya mamia ya mifano hai iliyoko katika historia ya kiislaam.

 

UISLAAM NI DINI YA HAKI NA KWELI

Lau kama wakiristo wange fahamu na kuelewa ya kuwa uislaam ni kweli na haki, na si matamshi tu bali ni matendo pia-kama ulivyo uislaam wa mtume (s.a.w.w), na uislaam wa Amiril-muuminiin Ali bin Abi Twalib (a.s)- je wasinge ingia kwenye uislaam? Vile vile Mayahudi kama wange swadikisha na kukubali kuwa huo ndio ukweli na uhakika wa uislaam, je suala lao lisinge ishia wao kuwa waislaam?

Je mfano huu hai pekee hautoshi kuwafanya wakiristo Mabuda na makafiri wengine wageuke na kuwa waislaam?

Vipi Mtume aliweza kuwabadilisha na kuwageuza watu wale, na kuwafanya kuwa waislam, hadi ikathibiti kauli ya Mwenyezi Mungu mtukufu: (Na utawaona watu wakiingia kwenye dini ya Mwenyezi Mungu makundi kwa makundi)? Kwa nini jambo kama hili jambo la (kuingia watu kwenye dini ya uislaam makundi kwa makundi) katika kipindi cha miaka kumi na tatu ambayo Mtume aliimaliza akiwa Makka tukufu baada ya kupewa utume mtukufu halikuthibiti, tofauti na hivyo ni kuwa suala hilo lilifanyika katika miaka tisa na miezi kadhaa ambayo Mtume (s.a.w.w) aliimali na kuishi  katika mji wa Madinatul-munawwaarah, kwani watu kwenye mji huo waliingia na kuipokea dini ya uislaam makundi kwa makundi?

Kwa Hakika Mtume (s.a.w.w) aliweza kufanya hivyo, kutokana na ukweli kuwa sababu na mazingira ya kuweza kulifanya hilo na kulifanikisha yalikuwepo.

Kwa hivyo basi mazingira kama hayo ikiwa yatapatikana kwa wote, katika sehemu yoyote ya ulimwengu, kukiwemo nchi na miji ya makafiri, na kutangaza jambo hili, na kutekelezwa kimatendo na kuonekana wazi wazi katika ardhi, kwa hakika watu wa sehemu zile na maeneo hayo wange geuka na kubadilika na kuingia kwenye uislaam.

Mtume (s.a.w.w) alikuwa ni mtu bora, na ni mtu alie kuwa na mfumo bora… sasa ninani asie penda kufuata mfumo ulio bora, au kujiunga na nidhamu iliyo safi na nzuri?!

Hakika utukufu na Izza ya kiutu, na dhamana au bima ya kijamii ambayo Mtume wa uislaam (s.a.w.w) liitekeleza na iliyo tekelezwa na Amiiril-muuminiin (a.s), hakuna mfano wake katika sehemu yoyote ya ulimwengu, kama ambavyo hakuna kanuni yoyote inayo lingana na kanuni za hali ya juu za kiislaam.

Hakika Aba dharril-ghafari alikuwa ni kijana wa kishirikina, sasa ni jambo gani lilimfanya kujiunga na uislaam? Ni kitu gani alicho kiona na kumfanya awe muislaam na mtu wa kupigiwa mfano? Na ni wingi ulioje wa athari alizo ziacha na kuzibakisha na zitakazo endelea kubakia milele na milele, kwani kuna mamia kwa mamia ya maulamaa wakubwa wa kishia, ambao ni matunda ya juhudi za Abi dharri radhi za alaah ziwe juu yake. Hawa waliona na kusadikisha pia kukubali.

 

MFUMO WA UTAWALA WA IMAMU ALI (A.S)

Kwa muda wa miaka kadhaa utawala wa kidunia na kidhahiri ulikuwa mikononi mwa Imamu amiriil-muuminiin (a.s), pindi alipokuwa katika mji wa Al-kuufah, na wakati huo Al-kufa ulikuwa ni mji mkubwa, na kutokana na yaliyo thibitishwa na kuandikwa na baadhi wa wanahistoria, ukubwa na upana wake ulikuwa ni zaidi ya kilo meta mia tano za mraba, na baadhi wamesema ya kuwa ukubwa wake ulikuwa ni zaidi ya hapo, na ulikuwa ni makao makuu na mji mkuu wa utawala wa Amiril-muuminiin (a.s).

Imepokelewa katika hali na historia ya Amiril-muuminin (a.s) ya kuwa katika muda wa miaka mine na miezi kadhaa, ambayo ndio miaka na muda wa utawala wake wa kidhahiri (a.s), kulitokea tukio na jambo moja na mara moja tu, historia haikutaja kutokea kwa tukio lingene kama hilo, na hakuna katika vitabu vingine habari ziashiriazo kuwa tukio kama hilo lilitokea na kujikairir katika utawala wa Imamu Ali (a.s).

 

BIMA YA KIJAMII KUONEKANA  KWA MARA YA KWANZA ULIMWENGUNI

Riwaya inasema ya kuwa siku moja Amiril-muuminiin (a.s) alikuwa akipita  na kuvuka katika moja ya barabara za mji wa Al-kuufah, akamuona mtu akinyoosha mkono na kuomba akasema: Ni kitu gani hiki? Baadhi ya watu waliokuwa hawafahamu ukweli na uhakika wa uislaam wakamjibu, kwa kusema: Huyu ni mkiristo… kwa hakika amezeeka na hana nguvu tena za kufanya kazi, kwa hivyo yeye anaomba !!

Na huenda yule mtu aliejibu alifikiria na kudhani ya kuwa suala linafoautiana kwa Amiril-muuminiin (A.S) ikiwa mwenye kuomba si muislaam, wakati ambapo katika kanuni ya kiislaam hakuna tofauti katika jambo hilo katika upande huu… watu hivi leo hawafahamu matukio kama haya, na huenda wasikubali na kuswadikisha matukio kama haya, na watasema: kwa nini waislaam wa leo hawako hivi na katika mfumo kama huu?

Lakini Imamu Amiril-muminiin (a.s) akaanza kuwalaumu maswahaba wake kutokana na tukio alilo liona la yule mkiristo, na akasema: Mmemfanyisha kazi hadi kufikia uzee na kutokuwa na uwezo wa kufanya kazi mkamnyimia mali zenu) (Shekh tuusiy: Tahdhiibul-ahkaam, juzu 6 / 293).

Mkiristo yeyote, au Yahudi yeyote, bali hata mtu yeyote mwenye kuabudu masanamu mkimuonyesha mfano hai kama huu, kisha asibadilike na kugeuka? Ikiwa atakubali na kusadikisha,  hapana budi atabadilika na kugeuka na kuathiri katika familia yake na kuifanya ibadilike pia.

Je kuna nchi yoyote katika dunia na ulimwengu wa leo ambayo haina  watu omba omba? Lau kama mtakwenda na kutembelea nchi tajiri kabisa ulimwenguni, mtawakuta mafukara na omba omba.. bila shaka yoyote, na jambo hilo linatofautina ukubwa wake nchi hadi nchi nyingine, kwani kuna nchi ambayo mafukara na omba omba huko ni wengi zaidi, na nchi zingine ni wachache.. na kuendelea, kwa hivyo nyinyi mtaona ya kuwa hata nchi zenye maendelea sana ulimwenguni, na zenye utawala na nidhamu na kanuni bora za zama hizi utakuta kuwa kuna omba omba,  wakati ambapo katika uislaam mas’ala kama haya hayahesabiwi kuwa ni mas’ala ya mtu binafsi, bali hakuna maana yoyote ya kuwepo omba omba katika nchi ya kiislaam!

 

UISLAAM NI KWA AJILI YA DUNIA NA AKHERA

Uislaam hauhusiani na akhera pekee.

Bali uislaam  unamaana ya: wema na saad ya dunia pia.

Uislaam  yaani ni Amani.

Uislam yaanin ni uchumi bora na salama.

Uislaam yaani ni siasa safi na bora.

Uislaam yaani ni Jamii safi na nadhifu.

 Uislaam yaani ni kila kitu kiwe sawa na salama.

Na Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.w) yeye mwenyewe,, wakati alipokuwa katika mji wa Madinatul-munawwarah, bali wakati alipokuwa katika mji wa Makkatul-mukarramah pia na wakati huo hakuwa ni mwenye uwezo mkubwa, alitangaza:

(Niitikieni na kujibu wito wangu mtakuwa wafalme duniani na akhera), na maana ya hayo ni kuwa njooni na muingie kwenye uislaam, ili mpate saada na wema wa duniani na akhera, yaani dunia itakuwa ni pepo kwenu, na katika akhera mwisho wenu utakuwa ni kuingia peponi pia.(Buharul-an’waar: juzu 18 / 185, h15).

Kama ambavyo uislaam wa Amiril-muuminiin (a.s), unamaana ya uislaam sahihi, yani uislaam wa kauli na matendo, na si uislaam wa jina pekee, kama alivyosema Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.w) kuhusiana na uislam na kuwa katika uislaam kutakuwa na watu (Umma wangu utapitiwa na kujiwa na zama ambazo hakutabakia katika uislaam isipokuwa jina lake) (Buharul-an’waar: juzu 36, 284).

Kutokana na hilo ndio maana Amiril-muuminiin (a.s) akaamuru kuhusiana na suala la mkiristo yule alie kuwa akinyoosha mkono na kuomba msaada, apangiwe mshahara wa kumtosheleza kuendesha maisha yake kutoka kwenye baitul-maali.

Ndio Mtume wa Uislaam (s.a.w.w) aliupatia ulimwengu zawadi hii ambayo ndani yake kuna saada na wema kwa viumbe na wakati atakapo dhihiri Swaahibuz-zaman walii mtukufu wa Mwenyezi Mungu Imamul-hujjah (Mwenyezi Mungu aharakishe kudhihiri kwake) hapo ahadi ya Mwenyzi Mungu itathibiti ile isemayo : Ili aidhihiridhe na kuipa ushindi dini yake juu ya dini zote) (Suuratul-baqarah aya 33), na hapo kutangaa bendera ya uislaam pande zote za dunia, na watu wote kuwa waislaam.

 

USIA MBILI KUHUSU  MATENDO MEMA

Hapa ninawapa ndugu zangu usia mbili, na ninataraji watafanya juhudi kuzitekeleza usia mbili hizo inshaa’allahu tala:

Usia wa kwanza: Ni usia ule ambao ulikuwa ukisisitizwa sana na kaka yangu (mheshimiwa Ayatullahil-udhmaa sayyid Muhammad  Al-huseiniy Al-shirazi Mwenyezi Mungu ayafanye mema malazi yake) wakati wote na kwa mara kadhaa, bali ndio usia uliotoka kwa Mwenyezi Mungu alie takasika kabla ya kuwaumba wanadamu: Nao ni kuwa kila mmoja wenu afanye juhudi za kuweka na kufanya majlisi na vikao vya Azaa na maombolezo, na wote kushiriki katika vikao ma najlisi hizo hata baada ya kumalizika kwa mwenzi wa Safar, na kwa muda wote wa mwaka, kwani juhudi hizi tukufu na zenye baraka hazitapotea hivihivi bure na hazipotea hata kama ni kiwango cha ncha ya sindano, na vitakuwa ni akiba yenu nzuri na kuandikwa pia kuthibitishwa kwenye kitbu cha matendo yenu, ishaa allahu taala.

Kwa hivyo basi baad ya kumalizika mwezi wa Safar, jaribuni kufahamu utukufu wa tawfiqi hii kubwa, na ninataraji mtausiana nyinyi kwa nyinyi au kati yenu kufanya hivyo, na kwamba kila mmoja miongoni mwenu-sawa awe ni mlezi wa familia na mwenye nyumba, au awe bado ni kijana mdogo-ni juu yake kujiwekea masaa mawili maalum au saa moja tu, au hata nusu saa, kwa ajili ya Imamu Abii Abdillahil-huseini (a.s).

Fanya majlisi na vikao vya Sayyidish-shuhadaa katika nyumba yako binafsi na anza katika mwezi wa Safar.

Na ikiwa mmoja wenu ni fakiri na hamiliki chochote, basi ajitahidi kufanya na kutekeleza mambo yalinganayo na hali yake ya kiuchumi, kama kuwasha mshumaa au kuwasha taa kwa jina la Imam Husein (a.s) kwa muda wa dakika kadhaa kila wiki, katikati ya watu anao ishi nao nyumbani kwake.

Na ikiwa mtapata nafasi bora zaidi, na kupata tawfiiq, basi waiteni majirani zenu na watu wenu wa karibu au jamaa zenu na waumini wengine katika jambo kama hili.

Fanyeni juhudi wiki yoyote isikupiteni bila ya kutajwa na kukumbukwa ndani ya majumba yenu msiba wa Imamu Husein (a.s) katika kufanya hivyo kuna baraka za dunia na Akhera.

Hata ukiwa mwanachama au kiongozi wa kikundi na Hai’ah ya huseiniyyah , na kufanyika vikao kila usiku na mchana, na majli za kumbukumbu ya msiba wa Abi Abdillahil-huseini katika kikundi na Hai’ah hiyo, basi usiache nyumba yako ibakie bila kuwa na taa iwakayo kwa jina la Imamu Husein. Fanya kila juhudi kuhakikisha jambo hili linafanyika, na fanya juhudi ili uweze kupata tawfiqi kama hii ya kidunia na akhera.

Hakika majlisi na vikao vya kumkumbuka Imam Husein (a.s) ndio kichwa cha unyuzi ambacho kiliunganisha na kinaunganisha na kuwafikisha kwenye tawfiqi nyingi na za aina mbali mbali.

 

NI JUU YENU KUWATILIA HIMA VIJANA

Usia wa pili: Wahifadhini na walindeni  vijana wenu na mabinti wenu, na fanyeni kila juhudi ili wawe waumini wenye kumuamini Mwenyezi Mungu na Mtume wake (s.a.w.w) na Ahli baiti wake (a.s). Na vyovyote watakavyo fikia katika itikadi zao. Si semi ya kuwa izidisheni nyinyi itikadi yao, bali andaeni mazingira na  sababu za kuyatekeleza na kuyafanikisha hayo.

Ni juu yetu kuwaelewesha vijana na watoto Mtume wa Uislam (s.a.w.w) na Ahlil-baiti wake (a.s), kwa namna na jinsi ambayo walijiarifisha wao wenyewe (a.s), na kwa njia ile ile ambayo iliarifishwa na kutambulishwa na Qur’an tukufu Shakhsia ya Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.w), na uhakika wa maimamu watwaharifu (a.s) na sio kupitia ibara na maneno yale  pungufu au yaliyoo pitukia ambayo hutoka kwa baadhi ya sehemu na watu walio potoshwa  sehemu zisemazo kwamba inakusudiwa kuinua daraja na maqamu ya maimamu watwaharifu (a.s) zaidi ya kiwango chao cha kawaida, au kuwashusha hadi kwenye nafasi iliyo duni kuliko cheo chao.

Haijuzu kuwanasibishia hata sifa moja ya Mwenyezi Mungu alie takasika na kuwanasibishia maimamu watwaharifu (a.s), wafahamisheni vijana ukweli na uhakika wa mas’ala ya ismah, na mas’ala ya elimu ya ghaibu, mas’ala ambayo huzingatiwa kuwa ni miongoni mwa mambo yasiyo na shaka na mambo ya hakika yahusianayo na cheo na nafasi ya maimamu maasumiin (a.s).

 

IMAM  SWAADIQ  (A.S) ANAJITENGA NA KUWAKANA WAZUAO UONGO

Inasimuliwa ya kuwa mtu mmoja aliekuwa amepotoka (aitwae Muhammad bin Miqlaas) na mwenye kuniya ya Abil-khattab, alikuwa akijionyesha kuwa ni muislaam, wakati ambapo kiukweli hakuwa muislaam, alijichanganya na maswahaba wa Imamu Swaadiq (a.s), na akawa akitaradadi kati yao kwa muda kadhaa, na baada ya kupita muda kadhaa alijifunza baadhi ya maneno.

Na baada ya kupita muda, akawa akijiarifisha yeye mwenyewe kwa watu ya kuwa yeye anamuwakilisha Imam Swadiq (a.s), na akitoa na kuzungumzia mas’ala fulani fulani. Siku moja alidai ya kuwa Imam Swaadiq (a.s) ndie Mwenyezi Mungu, na kwamba yeye (Abal-khattab) ni mtume wake (!!), na habari zake zilipomfikia Imam (a.s), alimlaani kwa nguvu zote, na Abil-khattab aliambiwa kwa mara kadhaa ya kuwa Imamu Swaadiq amekulaani, lakini yeye hakuwa akijali, na alikuwa kisema kuhusiana na hilo: Hili ni jambo lililo tengenezwa, hakika Imam kwa kupinga kwake kulaani anataka kutanguliza maslahi!!

Sasa anafanya nini Imamu Swaadiq (a.s) kuhusiana na mtu kama huyu? Mambo yote hayaendi kwa muujiza, bali hapana budi watu wafanyiwe mitihani, hakika muujiza huwa na kufanyika kwa kiwango cha kutimiza hoja, na kwamba kule tu kuwepo kwa imamu maasumu, yaani Imamu Swaadiq (a.s) ni kutimiza hoja, (ili aangamie mwenye kuangamia akiwa na ubainifu) (Suuratul-anfaal aya 42) na maadamu hakujakuwepo na (ubainifu) hapo kunakuwa na muujiza.

(Muhammad bin Miqlaas) alisafiri na kwenda Makkaatul-mukarramah kwa ajili ya ibada ya hija, mtu mmoja akaja kwa Imamu Swaadiq (a.s), na kusema kuwa: Ewe mtoto wa Mtume wa Mwenyezi Mungu! Ibnu Miqlaas amekwenda hija, na ulipo fika wakati wa kuvaa Ihraam katika Miiqaati alisoma labaika kwa jina lako. Riwaya inasema: Machozi yalichuruzi kutoka kwenye macho mawili ya Imamu Swaadiq (a.s), na uso wake kubadilika, kisha akainua mikono yake kuelekea mbinguni, na akawa akiomba kwa unyenyekevu na kumuelekea Mwenyezi Mungu  mtukufu na kusema: Ewe Mola wangu! Si mimi.. mimi nakuomba msamaha..! Ewe Mola wangu mimi naomba msamaha kwako.. na akirefusha kumuelekea Mwenyezi Mungu na kunyenyekea kwa Mwenyezi Mungu mtukufu.

Vema, hapa tunauliza: Ni yapi madhara ya kitendo cha (Muhammad nib Miqlaas) kwa imamu Swaadiq (a.s)? je Qur’an tukufu haikusema kuwa: (Na mtu hatabeba mizigo ya mtu mwingine) (Suuratul-anAm aya 164).

Hakika Imam Swaadiq (a.s) anaifahamu zaidi aya hii kuliko mimi na nyinyi, na kwamba (Muhammad bin Miqlaas) ndie alie sema kauli ile kuhusiana na Imam Swaadiq (a.s), na Imam (a.s) yeye mwenyewe hakuyasema hayo, na wala hakudai madai kama yale, sasa kwa nini imamu analia, na kwanini anatatizwa (a.s)? kisha je Mwenyezi Mungu alie takasika hafahamu vema ya kuwa imam hakusema hayo, wakati yeye anafahamu mambo ya siri na dhahiri? Kama ambavyo imam (a.s) anafahamu pia ya kuwa (mzigo wa mtu habebeshwi mtu mwingine)…

Hakika (Muhammad bin Miqlaas) ndie ambae  alifanya dhambi, wakati alipovaa ihram na kusoma labaika kwa jina la Imam Swaadiq (a.s). Na Mwenyezi Mungu alie takasika na mtukufu anafahamu  ya kuwa Imam Swaadiq (a.s) ndie imamu yule ambae wakati anapo taka kusema (Labbaika) hutetema na kutatizika na kupatwa na msikitiko, na mishipa na nyama zake hutetemeka, na wala ulimi wake haumsaidia katika kauli yake, kwa sababu yeye anafahamu ya kuwa anazungumza na Mwenyezi Mungu alie takasika… ama sisi tunasema (Labbaika) haraka sana, kwa sababu sisi hatufahamu maana yake kamili, kinyume na imamu Swaadiq yeye anafahamu kiukamilifu maana na makusudio ya neno (labbaika).

Na huenda baadhi ya watu walio kuwa mahala pale kwa Imam (a.s) walistaajabu kwa kuomba kwake istighfari na kunyenyekea kwake kwa kiwango na namna kama hii, na kustaajabu kwa hayo aliyo yafanya. Imam anasema (a.s) kumwambia Zaidi An-narsiy-ambae ni mpokezi wa Hadithi-: Haikuwa istighfari yangu  na unyenyekevu wangu kwa Mwenyezi Mungu mtukufu isipokuwa ni kwa sababu ya kutaka utulivu na istikrari (utulivu wa kaburini mwangu) (Mustadrakul-wasaail juzu 9, 198). Yaani ili niwe na matumaini na utulivu kaburini mwangu.

Sasa je kuna ihtimali ya kuulizwa Imam Swaadiq (a.s) kaburini ya kuwa: kwa nini ulisema hivyo? Bila shaka hapana, na Imam (a.s) yeye mwenyewe anafahamu ya kuwa hato ulizwa  swali kama hilo, sasa nini maana ya kauli yake (a.s) (ili niweze kuwa na utulivu kaburini mwangu?!).

Baadhi ya watu walidai pia ya kuwa Sayyid Masiih (a.s) ndie Mwenyezi Mungu, na Qur’an tukufu inaashiria na kuzungumzia ya kuwa siku ya kiama, na watu wakiwa katika uwanja wa hesabu na kupewa malipo yao kwa mujibu wa uadilifu wa Mwenyezi Mungu ulio mpana, sayyid Masihi ataulizwa akiwa mbele ya viumbe: (je wewe uliwambia watu ya kuwa nifanyeni mimi na mama yangu kuwa ni miungu kinyume cha Allah) (Suuratull-maaidah aya 116).

Hakika Mwenyezi Mungu alie takasika anafahamu ya kuwa Isa (a.s) hakusema vile, na huenda Mwenyezi Mungu alie takasika anataka kuwakemea wale walio toa madai yale ya batili kutokana na malengo na magonjwa yaliyomo katika nafsi zao.

Baadhi ya maulamaa wamesema ya kuwa: Huenda kuumia na kusononeshwa kwa imam Swaadiq (a.s) kutokana na matendo ya (Muhammad bin Miqlaas), na kuomba kwake istighfari na kunyenyekea kwake kwa Mwenyezi Mungu, na maana ya kauli yake (Ili niweze kuwa na utulivu kaburini mwangu) kulikuwa na maana ya kuwa: Mimi ninaomba istighfari na kunyenyekea kwa Mwenyezi Mungu, ili nisije kuambiwa kaburini mwangu ya kuwa:Je wewe ndie ambae ulisema kumwambia Muhammad bin Mqlaas, sema Labbaika kwa jina langu? Kwa hivyo Imam Swaadiq (a.s) hakutaka tu kuuliza swali kuhusiana na jambo hilo, kwa sababu yeye anatatizwa kuulizwa swali kama hilo.

Maneno kama haya yasiyo faa hayana maana yoyote, na mwenye kupitukia kwenye maneno hayo, na ambae huwanasibishia maimamu maasumiin (a.s)… maneno kama haya huwaudhi maasumiin, kwani wao ndio walio sema ya kuwa (Tuwekeni chini na tushusheni kunako cheo cha uungu) (yaani msitusifu na kutunasibishia cheo cha uungu) (Allum’atul-baidhaau 64).

Hakika kupitukia na kuvuka mipaka katika sifa, na kupitukia katika maneno, sio njia inayo faa ya kumfahamu Imam  maasumu (A.S), mfumo na njia kama hii huenda ukampelekea mwenye kufanya hivyo kulaaniwa na maasumu (a.s), huenda Imamul-hujjah (a.s) akamlaani mtu yule ambae anamfanya na kumjaalia pia kumuweka Imam maasumu (a.s) kwenye cheo na daraja ya juu kabisa kuliko cheo na daraja yake ya kweli.

Hakika sifa za uungu, ni sifa maalum na makhsusi tu kwa ajili ya Mwenyezi Mungu mtukufu pekee, na majina ya Mwenyezi Mungu mazuri au Asmaaul-husnaa yanahusiana na kuambatana na dhati ya Mwenyezi Mungu  mtakasifu pekee.

Imam amesema (a.s):(Wataangamia kwangu watu wawili: Mwenye kupenda na kupitukia mipaka, na mwenye kuchukia na kusema yasiyo stahili) (Buharul-anwaar: juzu 39 295).

 

KHAATIMA (MWISHO)

Kwa hivyo basi ni juu yenu kuwalinda na kuwahifadhi vijana… na huu ni wajibu wa akina baba na akina mama, baba wadogo na wajomba.. na jamaa wa karibu na familia, na ni wajibu wa vijana wenye kushikamana na dini pia.

Tilieni hima majlisi na vikao vya kidini na vitangazeni vikao hivyo, vile vile majaalisi na vikao vya kubmukumbu za Ahlil-baiti (a.s), na majaalisi za Qur’an, vile vile vikao vya masomo ya kidini ambavyo hufanyika kwa ajili  ya kubainisha misingi ya dini na matawi yake, na vibainishavyo kuhusu marejeo ya kiama na akhera, na vimuelezeavyo Mwenyezi Mungu mkubwa na wa juu.. ili itikadi sahihi ziweze kuhamia kwa watoto wa kiume na kike.

Kijana yeyote mnae mfahamu, mlindeni na kumhifadhi kwa njia yoyote iliyo sahihi,  na zungumzeni nae kwa njia na mfumo laini na ulio mzuri, na zoeeni kuzungumza nae kila mara.., na mkizungumza na kijana mara kama kumi hivi, na hakuvutika  kwenu, basi zungumzeni nae kwa mara ya kumi na moja, hadi mara ishirini na zaidi.. kilicho muhimu msikate tamaa, kwa sababu kila anapo potoka kijana basi historia yenyewe hubadilika na kugeuka.. na kila anapo amini kijana na akawa ni mwenye kuitakidi haki, yawezekana wakaongoka kupitia kwake katika siku za baadae maelfu ya vijana.

Ninasisitiza kwa mara nyingine juu ya usia mbili hizi:

Usia wa kwanza: Fanyeni majaalisi na vikao kila wiki kwa jina la Imamu Husein (a.s) majumbani mwenu.

Usia wa pili: Vijana ….vijana… walindeni na kuwahifadhi vijana hawa, na ilindeni itikadi yao..

Ninataraji, kwa baraka za Mtume wa Mwenyezi Mungu(s.a.w.w) na Ahlil-baiti maasumiin na watwaharifu (a.s) yakubaliwe matendo yenu nyote, na yaandikwe kwenye madaftari ya matendo yenu mema, na muwafikishwe wote kutekeleza usia mbili hizi

Na swala na salam ziwe juu ya Muhammad na jamaa zake walio watwaharifu.

Wal-hamdu lillahi rabbil-aalamiin.