KIFUNGU CHA KWANZA
USULUD-DIN (MISINGI YA DINI)

MISINGI YA DINI NI MITANO:
1-TAWHIID (Kumpw ekesha Mwenyezi Mungu)
2-AL-ADLU (Uadilifu wa Mwenyezi Mungu)
3-AN-NUBUWWATU (Utume)
4-AL-IMAMATU (Uimamu)
5-AL-MA’AAD (Marejeo ya kiama)
 

1-TAWHIID

(Kumpwekesha Mwenyezi Mungu)
Tawhiid: ni mwanadam kufahamu ya kuwa ulimwengu unae muumba alie uumba na kuufanya uwepo baada ya kuto kuwepo na ni mwenye kila kitu.. kama uumbaji, utoaji wa riziki na utoaji wa neema na mzuiaji mwenye kuhuisha na kufisha na mwenye kutoa swiha na ugonjwa… yote hayo yako chini ya utashi wake. Amesema mwenyezi Mungu mtukufu:

إنما أمرُهُ إذاأراد شيئا أن يقول له كن فيكون

(Hakika si jambo jingine pindi atakapo jambo au kitu chochote huliambai kuwa na likawa).
Na dalili juu ya kuwepo kwa Mwenyezi mungu mtukufu: Ni vitu tuvionavyo mbingu na vilivyomo ndani ya mbingu hiyo, kama jua lenye kuangaza na mwezi wenye kutoa nuru na nyota zenye kumeremeta na mawingu, pepo na mvua.
Pia Ardhi na vilivyomo ndani yake, kama Bahari, Mito, Matunda, Miti, madini ya aina tofauti na yenye thamani kama Dhahabu na fedha na Zamrad na mengineyo.
Na katika aina tofauti za wanyama wenye kupaa angani na wenye kuogelea majini na watembeao nchi kavu (yaani juu ya ardhi), wakiwa ni wa aina tofauti na wenye sauti zenye kutofautiana na ukubwa wenye kushabihiana (kufanana) na usio shabihiana.
Na mwanadamu wa ajabu mwenye hisia tofauti au mwenye viungo tofauti vya kuhisia kama kusikia, kuona, kunusa, kuonja, na kugusa na kuwazia na mwenye viungo vingi vingine, kama macho, masiko,ulimi, moyo, mikono miguu, afya, ugonjwa, maridhio, ghadhabu, huzuni, furaha na mengi mengineyo.
Yote hayo ni dalili juu ya kuwepo kwa mola mwenye hekima na mjuzi, tunamuitakidi na kumuabudu na kumtegemea kutupa usaidizi na kutawakali kwake.
 

MWENYEZI MUNGU MTUKUFU NA SIFA ZAKE NJEMA

Mwenyezi Mungu alie takasika anazo sifa nyingi kama:
ELIMU: Yeye ni mwenye kufahamu kila kitu, kikubwa na kidogo na anayafahamu yaliyomo ndani ya nyoyo.
UWEZO: Yeye ni mwenye uwezo juu ya kila kitu, ana uwezo wa kuumba, kutoa riziki, kufisha na kuhuisha na mengineyo.
UHAI: Yeye yu hai hafariki.
UTASHI: Yeye hukitaka kitu ambacho kina maslahi ndani yake na wala hakitaki kitu ambacho ndani yake kuna ufisadi au uharibifu.
KUDIRIKI: Yeye hukiona kila kitu na husikia kila sauti hata kama itakuwa ni kwa kunong'onezana masikioni au wahm (kufikiria).
UTANGU: Yeye Mwenyezi Mungu pekee ndie wa tangu na tangu na ndie wa milele, yaani yeye alie takasika alikuwepo kabla ya kila kitu kisha akaviumba vitu vyote na atabakia kuwepo baada ya vitu hivyo hadi milele na ulimwengu wote huu ni miongoni mwa uumbaji wake, au ni viumbe vyake, viumbe hivyo ni vyenye kumuhitajia si katika kupatikana kwake pekee bali katika kubakia kwake na kuendelea kuwepo kwa vitu hivyo pia, na kila kilicho umbwa basi kitu hicho ni chenye kuzuka, kwa hivyo basi hakuna wa tangu na tangu isipokuwa Mwenyezi Mungu mtukufu.
KUZUNGUMZA: Yeye Mwenyezi Mungu ni mwenye kuzungumza, humsemesha amtakae katika waja wake wema walio takasika na kutakaswa, mitume wake na malaika wake.
UKWELI: Yeye ni mkweli katika yale ayasemayo na hakhalifu ahadi zake (yaani haendi kinyume na ahadi zake), kama ambavyo yeye alie tukuka ni muumba, mtoaji wa riziki, muhuishaji, mtoaji, mzuiaji, mwenye huruma, msamehevu, mtukufu, mbora na mkarimu…………nk

 

MWENYEZI MUNGU AMETAKASIKA NA SIFA MBAYA
MWENYEZI MUNGU ALIE TAKASIKA NA KUTUKUKA AMEEPUKIKA NA SIFA ZA UPUNGUFU:

 Mwenyezi Mungu si mwenye kiwiliwili na wala si murakkab (yaani hakuunganika kwa sehemu tofauti)  hana sehemu wala mahala maalum.

Na haiwezekani kumuona Mwenyezi Mungu mtukufu, si katika Dunia wala Akhera, na wala hatokewi na mabadiliko, hapatwi na kiu, hashikwi na njaa,  hazeeki hamaliziki, hashikwi na mghafala wala kulala.

Na hana mshirika wala mwenza, bali yeye ni mmoja na wa pekee, mmoja mwenye kutegemewa, hana mke wala mtoto.

Na sifa zake ndio dhati yake yenyewe, hakuna uwili kati yake na sifa zake, yeye ni muweza mjuzi hadi mwisho wa sifa zake njema kuanzia tangu na tangu, si kama sisi, kwani tulikuwa ni wajinga kisha tukajifunza na hatukuwa ni wenye uwezo kisha tukawa ni wenye uwezo.

Na yeye ni ghanii (tajiri na mwenye kujitosheleza) na hakihitajii chochote na yeyote, hahitaji ushauri wa yeyote, au msaidizi au waziri, au askari na mfano wa hayo.